TRA YAJIPANGA KUKUSANYA ZAIDI YA SHILINGI TRILIONI 41 MWAKA MPYA WA FEDHA
Na Gladness Kowero
Arusha
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepewa lengo la kukusanya Shilingi trilioni 41 na bilioni 830 kwa Tanzania Bara na Zanzibar katika mwaka wa fedha ulioanza Julai Mosi, baada ya kukusanya Shilingi trilioni 37 na bilioni 960 katika kipindi cha miezi 12 iliyopita dhidi ya lengo la Shilingi trilioni 36 na bilioni 70, sawa na ufanisi wa asilimia 105 na ukuaji wa asilimia 17.
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amebainisha hayo wakati akifunga mkutano mkuu wa mwaka wa tathmini ya utendaji wa mamlaka hiyo jijini Arusha, akisema matokeo hayo yanaonyesha kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato na kuweka msingi wa kutekeleza lengo jipya la mwaka wa fedha .
Mwenda amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa walipa kodi, maboresho ya mifumo ya ukusanyaji wa mapato, matumizi ya teknolojia pamoja na juhudi za watumishi wa TRA katika kusimamia ukusanyaji wa kodi.
Amesema katika mwaka mpya wa fedha, TRA itaendelea kuimarisha na kurahisisha huduma kwa walipa kodi kupitia mifumo ya kidijitali, kupanua wigo wa walipa kodi na kuongeza matumizi ya takwimu ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.
Aidha, amesema maboresho mbalimbali yaliyofanywa na Serikali pamoja na utekelezaji wa sheria za kodi yataendelea kuweka mazingira bora ya biashara, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza mapato ya Serikali.
Mwenda amesisitiza kuwa mafanikio ya TRA yanategemea ushirikiano wa walipa kodi, sekta binafsi na wadau wengine, akiwahimiza wananchi kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari ili kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wa watumishi wa TRA, amewapongeza kwa mchango wao katika kufanikisha malengo ya ukusanyaji wa mapato, akieleza kuwa mamlaka hiyo itaendelea kuboresha mazingira ya kazi, kuimarisha motisha na kuwekeza katika mifumo ya kisasa ili kuongeza ufanisi na tija.
Amesema ushirikiano kati ya uongozi, watumishi na walipa kodi utaendelea kuwa msingi muhimu katika kufanikisha lengo la kukusanya Shilingi trilioni 41 na bilioni 830 katika mwaka wa fedha unaoendelea.





Comments
Post a Comment