SHULE ZANUFAIKA NA PROGRAMU YA KUJENGA UWEZO WA VIJANA KATIKA MAWASILIANO.


 Na Gladness Kowero Arusha 

Katika zama ambazo uwezo wa kuwasilisha mawazo, kujenga hoja na kufanya maamuzi sahihi unatajwa kuwa nguzo muhimu kwa viongozi wa kesho, programu ya Pan African Speech and Debate Dialogue imeibuka kuwa jukwaa linalowajengea wanafunzi ujasiri wa kuzungumza, kufikiri kwa kina na kushiriki mijadala yenye kuleta suluhisho kwa changamoto za Afrika.


Hayo yameelezwa na Mwanzilishi wa programu hiyo na Mwalimu shule ya sekondari Butimba kutoka Mwanza ,Godlove Shami, jijini Arusha wakati wa kuhitimisha mdahalo huo na kusema kuwa kupitia programu hiyo, vijana wanapata nafasi ya kujifunza namna ya kujenga hoja, kusikiliza mitazamo tofauti na kujiandaa kuwa viongozi watakaoweza kukabiliana na changamoto za kizazi cha sasa.

Kwa upande wa washirika kutoka Marekani akiwemo,Adam Thane [Coordinator in north America for pan African] amesema lengo kubwa la ushirikiano huo ni kuwasaidia vijana kuondokana na hofu ya kuzungumza mbele ya hadhara na kuwapa ujuzi wa mawasiliano unaohitajika katika elimu, ajira na uongozi.



Ameongeza kuwa uwezo wa kueleza mawazo kwa ufasaha na kujenga hoja zenye mantiki ni nyenzo muhimu kwa vijana wanaotarajiwa kuwa viongozi wa Afrika katika siku zijazo.




Naye mratibu wa [TELTA] Chama cha walimu wa kingereza Tanzania Bi Augustina Mtui amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha ameema imeandaa mkakati wa kuanzisha klabu za mijadala katika shule mbalimbali za mkoa huo ili kuhakikisha wanafunzi wengi zaidi wanapata fursa ya kukuza vipaji vyao katika eneo la mawasiliano na uongozi.


Amesema walimu kutoka shule 11 tayari wamepatiwa mafunzo ya kuwa walezi wa klabu hizo, hatua ambayo itasaidia programu hiyo kuendelea kuwa endelevu hata baada ya mashindano kumalizika.



Nao baadhi ya washiriki wa programu hiyo wamejadili mada mbalimbali ikiwemo faida na changamoto za Biashara Huria Afrika, huku waandaaji wakisisitiza kuwa kupitia mijadala, wanafunzi wanajengewa uwezo wa kufanya tafiti, kutumia teknolojia za kisasa, kufikiri kwa kina na kuwa viongozi wenye kujiamini katika karne ya 21.


MWISHO.

Comments

Popular posts from this blog

WATUMISHI NGORONGORO KUNUFAIKA NA MILIONI 500, WAONYWA MIKOPO KAUSHA DAMU.

UGANDA ELECTION COMMISSION CONTINUES RECEIVING RESULTS AS MUSEVENI TAKES EARLY LEAD

WANANCHI WA NGORONGORO WAIBUA WASIWASI KUHUSU MAPENDEKEZO YA TUME.