NGORONGORO, SIMBA SC WAUNGANA KUITANGAZA TANZANIA DUNIANI KUPITIA UTALII NA MPIRA

 




ARUSHA – 

Na Gladness Kowero 

Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) na Klabu ya Simba SC zimezindua ushirikiano wa kimkakati utakaotumia nguvu ya mpira wa miguu kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii duniani kupitia kampeni maalumu ya "Simba Visit Ngorongoro – The Pride Returns Home."

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Abdul-Razaq Badru amesema ushirikiano huo unaunganisha sekta mbili zenye mchango mkubwa katika uchumi wa taifa, utalii na michezo, kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi.

Badru amesema Simba ni moja ya chapa kubwa zaidi katika soka la Afrika Mashariki na Kati, huku Ngorongoro ikiwa moja ya vivutio vinavyotambulika duniani kutokana na urithi wake wa kipekee na hadhi yake ya kimataifa.

Amesema kampeni ya "The Pride Returns Home" itakuwa sehemu ya maadhimisho ya miaka 90 ya Klabu ya Simba na itasaidia kuhamasisha Watanzania na wageni kutembelea Hifadhi ya Ngorongoro, huku mapato yatokanayo na utalii yakiendelea kuchangia shughuli za uhifadhi na maendeleo ya taifa.


Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Zubeda Sakuru amesema klabu hiyo imeamua kusherehekea miaka 90 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1936 kwa kurejea "nyumbani", akieleza kuwa nembo ya Simba imekuwa sehemu ya historia ya klabu hiyo tangu kuanzishwa kwake.

Amesema kupitia Wiki ya Simba kutakuwa na shughuli mbalimbali zitakazofanyika Ngorongoro ikiwemo uzinduzi wa matawi, programu za kijamii na uzinduzi wa jezi mpya ya klabu, huku akiwataka Wanasimba duniani kote kushiriki maadhimisho hayo.


Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Simba SC, Crescentius Magori amesema ushirikiano huo utatoa fursa kubwa ya kuitangaza Ngorongoro kwa mamilioni ya mashabiki wa Simba wanaofuatilia klabu hiyo kupitia mitandao ya kijamii, akisisitiza kuwa hatua hiyo itanufaisha sekta ya utalii na uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA, Dkt. Harrieth Mtae amesema ushirikiano huo unaendana na maono ya kuifanya Ngorongoro kuwa kivutio cha utalii cha kiwango cha kimataifa na kuchangia utekelezaji wa vipaumbele vya taifa vya kukuza utalii, uchumi na diplomasia ya kimkakati.



Amesema kampeni hiyo pia itakuwa sehemu ya maandalizi ya Tanzania kuelekea AFCON 2027, akibainisha kuwa michezo imeendelea kuwa chombo muhimu cha kuitangaza Tanzania, kuhamasisha uhifadhi na kuvutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi.


Comments

Popular posts from this blog

WATUMISHI NGORONGORO KUNUFAIKA NA MILIONI 500, WAONYWA MIKOPO KAUSHA DAMU.

UGANDA ELECTION COMMISSION CONTINUES RECEIVING RESULTS AS MUSEVENI TAKES EARLY LEAD

WANANCHI WA NGORONGORO WAIBUA WASIWASI KUHUSU MAPENDEKEZO YA TUME.