WANANCHI NGORONGORO WATAKA MAJIBU YA HARAKA KUHUSU RIPOTI ZA TUME ZA RAIS.
WANANCHI NGORONGORO WATAKA MAJIBU YA HARAKA KUHUSU RIPOTI ZA TUME ZA RAIS.
ARUSHA
Wananchi wa jamii ya Wamaasai katika Wilaya ya Ngorongoro wameeleza wasiwasi wao juu ya kucheleweshwa kwa ripoti za tume mbili za Rais zilizoundwa mwezi Februari mwaka 2025 kuchunguza migogoro ya ardhi katika eneo hilo.
Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa Machi 5 mwaka huu, wananchi hao wamesema tume hizo zilipewa muda wa siku 90 kukamilisha kazi na kuwasilisha ripoti zake, ambapo zilitarajiwa kukamilika Mei 2025 lakini hadi sasa bado hazijatolewa.
Wananchi hao wanasema kucheleweshwa kwa ripoti hizo kumeibua hofu na taharuki miongoni mwao, huku wakisubiri kwa hamu majibu ya masuala waliyowasilisha mbele ya tume hizo ikiwemo changamoto za matumizi ya ardhi, huduma za kijamii pamoja na mpango wa serikali wa kuwahamisha wakazi kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda kijiji cha Msomera mkoani Tanga.
Aidha, wananchi hao wamedai kuwepo kwa vitendo vya kukamatwa kwa mifugo, kuvunjwa kwa nyumba na vikwazo vya upatikanaji wa maeneo ya malisho, wakihofia kuwa maoni yao yanaweza yasizingatiwe katika mapendekezo ya tume hizo.
Pia wameeleza kuwa uwekezaji unaoendelea wa hoteli katika eneo hilo bila ushirikishwaji wa jamii unachangia kuziba mapito ya wanyamapori na mifugo.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wa Ngorongoro wameiomba serikali kusitisha mpango wowote wa kuhamisha wananchi kutoka eneo hilo na kurejesha ardhi iliyochukuliwa kwa ajili ya kuanzishwa kwa Pori la Akiba la Pololeti.
Aidha, wameisisitiza serikali kuhakikisha maamuzi yote yanayohusu ardhi yanafanyika kwa kushirikisha wananchi na kuheshimu haki zao za msingi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mikataba mbalimbali ya kimataifa ya haki za binadamu.
Mwisho.







Comments
Post a Comment