WANANCHI WA NGORONGORO WAIBUA WASIWASI KUHUSU MAPENDEKEZO YA TUME.
Arusha
Wananchi wa jamii ya Wamaasai wilayani Ngorongoro, hususan Tarafa ya Sale, wameeleza wasiwasi wao kuhusu mapendekezo ya tume mbili za Rais zilizowasilishwa hivi karibuni, wakihofia huenda zisitoe suluhisho la changamoto zinazowakabili.
Kupitia tamko lao la Machi 20, 2026, wananchi hao wanasema baada ya kuchambua ripoti hizo, wamebaini kuwa hazijaakisi kwa kina uhalisia wa maisha yao wala kuzingatia maoni waliyowasilisha wakati wa ukusanyaji wa taarifa.
Wanasema kwa muda mrefu wamekuwa wakiishi ndani ya mfumo wa ikolojia wa Ngorongoro na Serengeti kwa kutegemea ufugaji, wakiamini kuwa mfumo huo umewezesha kuendelea kwa uhifadhi wa mazingira kwa vizazi vingi.
Hata hivyo, wananchi hao wameeleza kuwa bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa maeneo ya malisho, ukamataji wa mifugo pamoja na vikwazo katika upatikanaji wa huduma za msingi.
Aidha, wameeleza kuwa mapendekezo yanayohusu kuendelea kwa uhamishaji wa wananchi kutoka katika maeneo yao yameibua hofu zaidi, wakisisitiza kuwa wanahitaji kushirikishwa kikamilifu katika maamuzi yanayohusu maeneo hayo ya uhifadhi.
Katika hatua nyingine pia, wamezungumzia umuhimu wa maeneo kama Ziwa Natron na Engaresero, wakibainisha kuwa mbali na thamani yake kiuchumi, maeneo hayo yana umuhimu wa kiutamaduni na kiimani kwa jamii ya Wamaasai.
Wananchi hao pia wameomba serikali kuzingatia maoni yao, kusitisha hatua zinazoweza kuathiri maisha yao, na kuhakikisha kuwa haki zao za msingi zinaheshimiwa katika mchakato mzima wa kutafuta suluhisho la mgogoro wa ardhi.
Wamesisitiza kuwa wako tayari kushirikiana na wadau mbalimbali ili kupata suluhisho la kudumu litakalolinda maslahi ya jamii pamoja na mazingira.
Mwisho





Comments
Post a Comment