SERIKALI YAIMARISHA MIUNDOMBINU YA AFYA ARUSHA, YAAGIZA UJENZI WA GOROFA KITUO CHA AFYA KALOLENI.

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha miundombinu ya utoaji wa huduma za afya nchini, ambapo Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ameziagiza mamlaka za Halmashauri ya Jiji la Arusha kuanza mara moja ujenzi wa jengo la gorofa katika Kituo cha Afya Kaloleni ili kukabiliana na msongamano mkubwa wa wagonjwa.

Waziri Mchengerwa ametoa maagizo hayo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utoaji wa huduma za afya katika kituo hicho, akisema idadi kubwa ya wananchi wanaohitaji huduma imekuwa ikiongezeka, hali inayosababisha changamoto katika utoaji wa huduma kwa ufanisi.

Amesema ujenzi wa jengo la gorofa utasaidia kuongeza wigo wa huduma, kuboresha mazingira ya kazi kwa wahudumu wa afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati na kwa ubora unaostahili.



Katika hatua nyingine, Waziri Mchengerwa amesifu jitihada za watoa huduma wa afya katika Kituo cha Afya Kaloleni, akiwemo Mganga Mkuu wa kituo hicho, kwa kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa weledi licha ya changamoto za miundombinu.

Aidha, Waziri Mchengerwa ametoa maelekezo ya utekelezaji wa sera na miongozo ya Serikali kwa kuhakikisha huduma zote za dawa zinapatikana ndani ya kituo hicho, akisisitiza kuwa hakuna mgonjwa anayepaswa kupelekwa kununua dawa nje ya kituo cha afya.

Amesisitiza pia umuhimu wa uwajibikaji, maadili na utu kwa wahudumu wa afya, akiwataka kuzingatia mawasiliano mazuri na kutumia lugha yenye heshima kwa wagonjwa, kwani huduma bora hujengwa kwa misingi ya taaluma na utu.

Waziri Mchengerwa amesema endapo ujenzi wa kituo hicho cha afya utakamilika kwa kuzingatia viwango na miongozo iliyowekwa, Serikali itaendelea na hatua za kukipandisha hadhi Kituo cha Afya Kaloleni kuwa Hospitali ya Wilaya, kutokana na uwezo wake wa kutoa huduma muhimu na uwepo wa vifaa vya kisasa.


Mwisho

Comments

Popular posts from this blog

WATUMISHI NGORONGORO KUNUFAIKA NA MILIONI 500, WAONYWA MIKOPO KAUSHA DAMU.

UGANDA ELECTION COMMISSION CONTINUES RECEIVING RESULTS AS MUSEVENI TAKES EARLY LEAD

WANANCHI WA NGORONGORO WAIBUA WASIWASI KUHUSU MAPENDEKEZO YA TUME.